Somo la Kwanza: Mdo 2:14, 22-33;
Somo la Pili: 1 Pt 1:17-21
Injili: Lk 24:13-35
Somo la Kwanza: Mdo 2:14, 22-33;
Somo la Pili: 1 Pt 1:17-21
Injili: Lk 24:13-35
Utangulizi
Kristo mfufuka anatembea pamoja nasi katika safari yetu ya maisha. Yeye ndiye anayetufunulia neno lake na kujifunua katika Ekaristi. Anatualika kukaa karibu naye na kuwa mashahidi kwa jirani zetu. Kurudi Yerusalemu.
Homilia
Somo la I: Katika somo la kwanza mtume Petro anawahubiria Wayahudi ukweli wa Mpango wa Mungu katika wokovu wetu unaotimia katika Kristo kwa kifo na ufufuko wake. Petro anasimama kwa ujasiri na kutangaza ukweli wa Yesu Kristo. Kwamba aliangukia mikono ya wabaya na yeye akakubali mpango wa Mungu utimie.
Tumwombe Mungu atujalie kutambua mpango wake hata katika mazingira ambayo hata sisi hatuelewi na kuyatambua.
Somo la II: Mtume Petro anatuhimiza tuishi maisha ya matakatifu tukikumbuka kwamba tumekombolewa si kwa vitu vya dunia bali kwa Damu ya Kristo. Tumekombolewa kwa gharama kubwa.
Petro anawakumbusha Wayahudi mintarafu sisi pia kwamba Mungu ni hakimu asiye na upendeleao. Hivyo tunapaswa kuishi katika hofu ya Mungu. Tumekombolewa kwa damu ya Kristo, aliyejitoa kama mwanakondoo asiye na doa. Hivyo maisha yetu hayawezi kuwa ya kawaida tena. Tugeukie Yerusalemu, tumgeukie Mungu, tusiuharibu ubatizo wetu tena kwa dhambi. Tumekombolewa kwa gharama kubwa.
Injili: Katika somo la Injili tumeona wanafunzi wanaenda Emau wakiwa na mashaka mioyoni mwao, wakiwa katika kusikia tu, wanarudi Yerusalemu wakiwa na furaha na Imani. Hii ni baada ya kufunuliwa mafumbo ya wokovu na Yesu kupitia maandiko matakatifu na kwa kuumega mkate wanafumbuliwa macho yao ya imani.
Yesu anatembea nasi kila mahali, ama Yesu yupo nasi kila mahali kwa kuwa kwa kufufuka kwake hafungwi tena na mahali wala na nyakati. Hata katika maisha yao ya kawaida wanafunzi hawa wanatembelewa na Yesu na wanafanikiwa kumtambua kwa kumpa nafasi ya kusikiliza neno lake na kuumega mkate.
Pia katika mashaka na wasiwasi na kutokuamini Yesu anatutoa huko. Yesu anawakomboa hawa wanafunzi wa Emau kutoka katika mashaka na kutokuamini kwao. Yesu anawafumbua macho yao ya kiimani. Mruhusu Yesu kwa kusikiliza na kusoma neno lake na kwa kushiriki Ekaristi Takatifu.
Neno la Mungu hufungua mioyo yetu. Yesu alipoanzia kuwafundisha neno lake aliwafungua mioyo yao. Aliwaonyesha jinsi maandiko yote yalivyomwelezea yeye. Mioyo yao ilianza kuwaka. Hii ni ishara ya uwepo wa Mungu katika maandiko matakatifu kupitia Roho wake Mtakatifu.
Uwepo wa Yesu katika kuumega mkate. Yesu anajidhihirisha katika kuumega mkate. Na hapa sio mioyo yao tu ilifunguliwa bali hata na macho yao kabisa wakamwona Yesu. Katika Ekaristi Takatifu Kristo anajitoa kwetu. Ni mahali pa kukutana na Yesu kwa namna ya Pekee kabisa. Na baada ya kumtambua walirudi Yerusalemu. Ukaribu na Mungu uandhihirishwa zaidi katika sakramenti ya Ekaristi Takatifu.
Hivyo ndugu wapendwa katika dominika hii, tumruhusu Yesu atembee nasi katika maisha yetu, atufunulie na kulitafakari neno lake kupitia Roho Mtakatifu. Kushiriki Ekaristi kwa Imani na kuwa mashahidi wa matumaini ya ufufuko wa Yesu kwa wengine. Turudi Yerusalemu kwa furaha na imani.
***************Bwana amefufuka kweli Alleluya Alleluya***********