Wito Hujifunua Katika Kuishi

2026-04-26
Dominika ya 4 ya Pasaka
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Mdo 2:14, 36-41;

Somo la Pili: 1 Pt 2:20-25

Injili: Yn 10:1-10

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Karibuni wapendwa katika Kristo, leo tunaadhimisha Dominika ya Yesu Kristo Mchungaji Mwema. Ndie mwenye dhamana ya maisha yetu, anajua kula yetu, kulala kwetu, kuamka kwetu kuenenda kwetu. Tuweke Tumaini letu kwake. Pia ni siku ya kuombea miito mitakatifu, ndoa, utawa na upadre. Yesu anaendelea kutuchunga sisi kupitia wachungaji wetu. Tumwombe Yeye aliye Bwana na Kristo tuweze kufuata nyayo zake kiamninifu kama Wakristo.

Homilia

Katika Dominika ya leo Yesu anajitambulisha kwetu kama Mlango wa Kondoo. Yeye ndiye bawabu, hinge, ya kuingia kwetu na kutoka kwetu. Kuingia wapi katika neema ya Pasaka, katika mlango wa Mbingu. Hivyo tukitaka kufika Mbinguni – pitia kwa Yesu, Ukitaka kufanikiwa pitia kwa Yesu, ukitaka kufauli pitia kwa Yesu, ukitaka neema pitia kwa Yesu. Ukitaka uzima nenda kwa Yesu.

Somo la I:  Katika somo la kwanza tunasikia Petro anafumbua kinywa chake na kuwafundisha Wayahudi kwamba, Mungu amemfanya Yesu huyo ambae mlimsulubisha kuwa Bwana na Kristo. Bwana: ikionyesha umungu wake na umoja na Mungu. Kristo: ikionyesha mpakwa, masiha, Mkombozi. Kwa maneno mengine Mungu amemfanya mchungaji wenu. Na mkitaka kuwa kondoo wake tubuni na mkabatizwe. Mtapata ondoleo la dhambi na mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

     Kwa ubatizo wetu ni kwamba tunakubali kuwa Yesu ni Bwana wa mwokozi wa Maisha yetu. Tunachotakiwa ni kufuata nyayo zake na kijikabidhi chini ya ulinzi wake dhidi ya maadui zetu wa kiroho na kimwili.

Somo la II: Katika somo la pili tunakutana tena na Petro anayewaimarisha Wakristo wa Mwanzo kuwa Kristo amewaachia kielelezo, na wanapaswa kufuata nyayo zake. Kwa kutokutenda dhambi, kwa kutokulipiza kisasi, kwa kutokuogopa bali alijikabidhi kwa Mungu. Nasi kama wakristo hatuna budi kujikabidha kwake. Na kama kondoo wake tukimfuata kwa hakika katika malisho ya majani mabichi atatulisha, atatuliza njaa yetu ya Kumfikia Mungu, na kando ya maji ya utulivu huniongoza; ishara ya Roho Mtakatifu anayetuongozo katika uzima wa milele.

Injili: Katika somo la Injili tunakutana na Yesu mlango wa zizi, Bawabu ya mlango, sauti ya kondoo, mchungaji wa kondoo na huwatangulia kondoo, mlinzi wa Kondoo, na yeye ndiye anayefahamu malisho sahihi ya kondoo. Yesu ndiye anayeita. Yesu ndiye anayetuongoza katika wito wetu.

     Katika maisha yetu Mungu anatuita kwa namna mbalimbali. Pia anatupa uhuru wa kuchagua kile tunachotaka kuishi katika yeye. Ndio maana wengine wanachagua maisha ya Ndoa, kuwa na familia ambapo ni mpango wa Mungu, weingine maisha ya utawa, kuishi kwa ajili ya kumpendeza Mungu kwa kumwekea Mungu nadhiri, wengine maisha ya upadre kwa kuweka pia nadhiri na viapo katika kumtumikia Mungu katika kanisa lake. Lengo letu sote ni kuunganika na Kristo. Kuendea utakatifu na ndio maana wito wowote unapata maana yake katika kuishi wito huo. Hivyo;

     Wito wa Mungu huanza kwa toba ya kweli: Tukirejea somo la kwanza tunapojiuliza nasi tufanye nini kutambua wito wetu wa kweli; jibu ni tubu na ubatizwe. Maana yake ni kwamba wito huanza kwa uongofu wa moyo.

     Kristo ndiye Mchungaji anayetualika tufuate nyayo zake. Aliyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake. Aliteswa, akafa na akafufuka ili atukusanye sisi katika zizi lake kupitia yeye aliye mlango wa zizi. Ni mfano na kielelezo cha wito wa aina yoyote, kujitoa kwa upendo kwa ajili ya wengine. Ukaribu na Mungu utufundisha upendo wa kujitoa.

     Yesu ndiye mchungaji mwema anayewajua watu wake. Mungu hatuoni kama kundi tu, bali anatufahamu kwa majina kila mtu. Yesu anawajua kondoo wake na majina yao. Yesu anakufahamu kwa jina. Anajua kula yako, vaa yako, kuingia na kutoka kwako; kazi kwako ni moja tu, trust Him and follow Him.

     Kristo ndiye mlango wa wokovu na uzima wa milele. Ili tuweze kutimiza malengo ya wito wetu hatuna kufungamana maisha yetu na Kristo. Tusipofungamana naye tutapotea na kuliwa na mbwa mwitu walio adui wa kondoo. Mbwa mwitu hao ni sauti nyingi za ulimwengu zinazopingana na maisha ya ukristo na wito tuliouchagua. Hivyo wito ni kuisikiliza na kuitikia sauti ya Mungu.

     Hivyo ndugu zangu tunaalikwa katika dominika ya leo kuisikiliza sauti ya Mungu, kuwasaidia na kuwaombea wengine hasa vijana katika kuitikia sauti ya Mungu, kuishi maisha ya kujitoa kwa ajili ya wengine. Tupafanye pale tunapoishi pawe vitalu vya miito mitakatifu. Wito ni zawadi ya Mungu kwetu. Tuilinde na tuiishi kwa imani hiyo zawadi kwa kujitoa kwake.