Tambua Nguvu ya Roho Mtakatifu Ndani Mwako

2026-05-10
Dominika ya 6 ya Pasaka
Pd. Nicas Mrosso, OFMCap.
📖 Masomo ya Dominika

Somo la Kwanza: Mdo 8:5-8, 14-17

Somo la Pili: 1 Pet 3:15-18

Injili: Yn 14:15-21

🕊️ Tafakari ya Neno

Utangulizi

Kristo aliyefufuka anaendelea kukaa nasi katika maisha yetu kwa njia ya Roho wake. Roho huyo hutenda kazi pamoja nasi. Sharti ni mojo tu kumpenda Kristo na kuzisika amri zake. Tumwombe Mungu atujalie imani ya kumpokea Roho wa kweli na kumruhusu afanye kazi ndani yetu.

Homilia

Ndugu wapendwa Yesu anawaandaa wanafunzi wake kumpokea Roho Mtakatifu, Roho wa Kweli ambaye atakuwa na wanafunzi wake katika kutenda kazi ya Mungu. Roho mtakatifu ndiye analifanya kanisa kuwa hai, ndiye anayetufanya kuwa hai.

Somo la I: Katika somo la kwanzia, Filipo, mmoja wa wale mashemasi waliochaguliwa anahubiri Injili huko Samaria. Injili inaenea nje ya Samaria Kanisa la mwanzo linakuwa na kuenea kwa mataifa. Filipo anafanya miujiza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyempokea. Anatoa pepo na kuonyesha ukuu wa Mungu. Wasamaria wengi wanaamini na wanabatizwa matokeo ya Injili ya Kristo kwa watu wote. Petro na Yohane wanaenda kuwawekea mikono na kuwaombea Roho Mtakatifu Wakristo wapya.

     Tunaalikwa kutambua na kuona kazi ya Roho Mtakatifu katika kanisa na katika wakristo. Roho Mtakatifu anatufanya kuwa na muunganiko hai na Mungu na kuushinda ulimwengu na pepo wachafu.

Somo la II: Katika somo la pili ndugu wapendwa, barua ya kwanza ya Mtume Petro inawatia moyo wakristo wa mwanzo waliokuwa wanapitia magumu ya kukataliwa na kuudhiwa kwa sababu ya Injili. Wanaalikwa kuwa na hekima na Imani katika magumu wanayopitia. “Ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndio mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.” Msimamo huu ndio msingi wa imani ya wakristo katika kuishi imani kwa kufuata dhamiri zetu njema zinazoongozwa na Roho wa Mungu.

     Somo hili linatutia nguvu kuhubiri imani yetu hata katika mazingira magumu. Kushuhudia imani yetu kwa matendo na mienendo yetu hata katika magumu na majaribu.

Injili: Somo la Injili linaturudisha wakati wa Karamu ya Mwisho ambapo Yesu anawaandaa wanafunzi wake kubaki imara na kumtegemea Roho Mtakatifu. Yesu anawapa ahadi ya Roho Mtakatifu ambaye atawafundisha na kuwakumbusha mafundisho yake. Yesu anawakumbusha pia kuhusu kuzishika amri zake ambapo ndio namna ya kudhihirisha upendo kwa Kristo. Na tatu Yesu anaahidi kuwa nao katika katika kuihubiri Injili. Hatawaacha yatima. Hii inadhihirisha uwepo wake kwetu kwa njia ya Sakramenti zake na kwa nguvu ya Roho mtakatifu. Katika masomo ya leo tunajifunza mambo yafuatayo;

     Upendo wa kweli unajidhihirisha katika kizishika amri zake. Kristo anasema mkinipenda mtazishika amri zangu. Imani yetu kwa kristo inaonekana katika kuzishika amri zake.

     Hatujaachwa yatima. Tunashuhudia uwepo wa Kristo katika maisha yetu kupitia Sakramenti zake. Na ushuhida wake unajidhihirisha katika neema na baraka tunazozipokea katika maisha yetu.

     Zawadi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Yesu ametuahidia Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Roho ambaye anapewa majina kama msaidizi, mfariji. Ndiye daima anayetuongoza na kutuwezesha kudumu katika kuhubiri Injili, kuishi imani yetu na kutoa ushuhuda wa Imani Yetu kwa wengine.

     Matokeo na ushahidi wa Roho Mtakatifu katika maisha yetu, imedhihirishwa katika somo la kwanza. Pepo wachafu wanatoka, viwete wanatembea na wagonjwa wanapona.

     Pia ujasiri katika ushuhuda wa imani. Katika somo la pili Mtume Petro anaonyesha namna ambavyo wakristo baada ya kupokea Injili wanavyopaswa kuwa jasiri wa imani na matumaini hata katika mateso.

     Roho Mtakatifu anazifanya dhamiri zetu kuwa hai. Katika somo la pili Petro anasisitiza kuwa “Ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema kuliko kutenda mabaya.” Hiyo ndio kuenenda kwa upole na kwa hofu ya Mungu.

     Hivyo, ndugu wapendwa tunaalikwa kumwomba Mungu atujalie kama Wakristo kutambua nguvu ya Roho Mtakatifu ndani mwetu na kuishi ushuhuda wa imani yetu kwa maneno na matendo. Tusiogope Kristo yupo nasi katika Sakramenti zake. Na hata katika magumu msaidizi na mfariji wetu yupo.